Nenda kwa yaliyomo

Imamu Ridha (a.s) na urithi wa kiti cha uongozi

Kutoka wikishia

Urithi wa uongozi wa Imamu Ridha (as) (Kiarabu: ولاية العهد للإمام الرضا (ع)) unaashiria kuteuliwa Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi wa Khalifa Maamun Abbasi, ambalo ni tukio muhimu sana katika maisha ya Imamu Ridha kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kukubali Imamu Ridha cheo cha kuwa mrithi wa uongozi wa Maamum mbali na kuwa ni suala la changamoto katika historia ya Uislamu, lina umuhimu kwa upande wa teolojia. Kwa mujibu wa Seyyed Jafar Murtaza Amili, mwanahistoria wa Kishia, hadithi mutawatir zinaonyesha juu ya kutoridhia na kukubali Imamu Ridha cheo hicho kwa kulazimishwa. Kwa maana kwamba, hakuwa ameridhia lakini alilazimishwa kufanya hivyo.

Maamun alipendekeza ukhalifa kwa Imam kabla ya urithi wa ukhalifa, na wakasema kwamba lengo lake lilikuwa ni kuimarisha ukhalifa wake. Lakini pamoja na kukataa pendekezo la Maamun, Imam Ridha alihoji uhalali wa ukhalifa wa Maamun. Kwa kutoukubali ukhalifa, Maamun alimlazimisha kuukubali ukhalifa kwa kutishia kumuua Imamu Ridha (as). Kwa hiyo, ilimbidi Imamu alikubali pendekezo la Maamun; lakini aliweka sharti la kutoingilia masuala ya serikali. Hali hiyo ya kulazimishwa na kutenzwa nguvu iliendelea katika hatua zote nyingine alizofanya na mara zote alikuwa akisema, mimi nimetishiwa kuuawa ndio maana nimekubali kuwa mrithi wa kiti cha uongozi.

Aidha wakati alipopendekezewa jambo hilo alitoa masharti kwamba hayuko tayari kutoa amri kwa mtu yeyote yule, wala kuzuia kutendeka jambo lolote lile, wala asitoe fatwa na hukumu za kisheria kwa mtu yeyote yule na wala asimuuzulu wala kumteua mtu yeyote yule. Hivyo ni jambo lililo wazi kuwa, ukitoa anwani ya kulazimishwa kukubali jina la mrithi wa kiti cha uongozi, Imamu Ridha (as) hakushiriki kwa namna yoyote ile katika matendo yote ya utawala wa Khalifa Maamun.

Yote hayo yalionesha kuwa alitenzwa nguvu kukubali pendekezo hilo, kwani mtu asiye na nafasi katika jambo lolote lile, hawezi kuwa mfuasi wa utawala husika. Khalifa Maamun naye alitambua vyema jambo hilo na alifanya kila ujanja kuhakikisha kuwa Imam Ridha (as) anajihusisha na masuala ya utawala, lakini Imam alikataa. Baadhi ya malengo ya Maamun kwa kitendo hiki yametajwa kama ifuatavyo:

  1. Kusalimika na hatari ya Imamu.
  2. Kumuweka chini ya uangalizi wake.
  3. kunyamazisha mapinduzi ya Maalawi.
  4. Kumtumia Imamu kuhalalisha ukhalifa wake.
  5. Kuwaridhisha watu wa Khorasan.

Kwa upande mwingine, baadhi wanaamini kwamba Fadhl bin Sahl alitengeneza mpango wa urithi wa uongozi wa Imamu Ridha kwa ajili ya kufikia ufalme wa Iran. Hata hivyo, wanasema kwamba Imam (as) aliweza kuwazuia kufikia malengo yao kwa sera na shughuli zake.

Kwa amri ya Maamun, Imamu Ridha alihamishwa kutoka Madina hadi Khorasan mwishoni mwa mwaka wa 200 Hijiria. Maamun alichagua njia ya safari hiyo kwa namna ambayo asingepitia miji ya wakazi ambao ni Mashia. Imamu Ridha alisimulia na kubainisha hadithi ya Silsilat al-Dhahb akiwa njiani kuelekea Neishabur. Katika Ramadhani ya mwaka 201 Hijria, Ma'mun alifanya hafla ya kuteuliwa Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi. Kwa muktadha huo, watu na maafisa wa serikali walitoa kiapo cha utii kwa Imam. Baada ya hapo, kwa mujibu wa amri ya Maamun, khutba zilisomwa kwa jina la Imamu na sarafu zilichongwa zikiwa na jina lake.

Kwa kutangazwa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as), watu kama Ali bin Abi Imran, Abu Yunus na mtawala wa Basra walipinga vikali jambo hilo. Watu wa Baghdad, ambao waliogopa kwamba ushawishi wao katika serikali ungepungua, waliasi na kula kiapo cha utii kwa Ibrahim bin Mahdi. Kwa mujibu wa vyanzo vya Shia, Imam Ridha (as) aliweza kutumia hali hiyo kwa maslahi ya Shia. Alieleza na kubainisha mafundisho mengi ya Ahlul-Bayt (as) kwa umma, na kufanaya mijadala na midahalo na viongozi wa madhehebu tofauti. Kulingana na baadhi ya watafiti, urithi wa kiti cha uongozi wa Imam Ridha (as) uliandaa uwanja na mazingira ya Wairan kuwa Mashia.

Umuhimu wa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha katika Uislamu

Suala la Imamu Ridha (as) kuwa Mrithi wa Kiti cha Uongozi ni mojawapo ya masuala yenye mjadala mkubwa katika historia ya Uislamu, [1] ambayo ni muhimu kisiasa na kiteolojia (kupingana kukubali urithi wa kiti cha uongozi na suala la Imamu kuwa Maasumu) [2] [3]. Kipindi cha Imamu Ridha cha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi wa Maamun kinahesabiwa kuwa kipindi muhimu zaidi cha maisha yake ya kisiasa. [4]

Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, katika kipindi nyeti cha cha ukhalifa wa Maamum, hatua ya Imam Ridha (as) ya kukubali cheo cha mrithi wa kiti cha utawala na wakati huo huo kufanya harakati katika kipindi hicho aliweza kuiongoza jamii kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwani katika wakati huo, utawala wa ukoo wa Bani Abbas ulikuwa ukikabiliwa na hali isiyo thabiti na kulikuwa na uasi mwingi wa Maalawi sambamba na kuweko baadhi ya makundi potofu ambayo yalikuwa yameandaa mazingira na anga ya jamii kusambaratika. [5]

Pendekezo la cheo cha urithi wa kiti cha uongozi

Kwa mujibu wa Abul Faraj Esfahani katika Maqatil al-Talibiyyin na Sheikh Sadouq katika kitabu Uyun Akhbar al-Ridha (a.s.), urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha ulifanyika na kutimia kwa takwa la Maamun; kwani yeye alikuwa amekula kiapo kwamba, endapo atamshinda nduguye yaani Amin ataukabidhi ukhalifa kwa Imamu Ridha. [6] Baada ya Amin kuuawa na utawala ukawa mikononi mwa Maamun, Sahl bin Fadhl waziri wa Maamun alimkumbusha ahadi aliyofunga na Mwenyezi Mungu na hivyo Maamun akachukua hatua za lazima, kwa ajili ya jambo hilo. [7]

Kwa upande mwingine, baadhi ya watu wanaamini kwamba pendekezo la urithi wa kiti cha uongozi kwa Imam Ridha lilitolewa na Fadhl bin Sahl. [8] Inasemekana kwamba, kwa hatua hii Fadhl alitaka kufikia ufalme wa Iran baada ya Imamu Ridha (as). [9] Kuteuliwa kwa Raja bin Abi al-Dhahhak ambaye ni katika jamaa wa Fadhl bin Sahl na kupewa jukumu la kumhamisha Imam Ridha kutoka Madina hadi Merv, onyo la baadhi ya wanasiasa kwa Maamun kuhusu mpango wa Sahl na ripoti nyingine za kihistoria zinazingatiwa kama uthibitisho wa dai hili. [10]

Malengo

Ingawaje kuna baadhi ya wanazuoni wa Kimagharibi (watafiti wa masuala ya Mashariki) pamoja na wachambuzi kadhaa wa Kishia, akiwemo Hassan Amin wa Lebanon, waonadai kuwa Ma'mun alikuwa na nia njema katika uteuzi huo wa kumteua Imamu Ridha (a.s) kama ni mrithi wake. [11] Ila, idadi kubwa ya watafiti inashikilia Imani isemayo kuwa; uteuzi huo ulikuwa ni mkakati wa kisiasa uliolenga kufikia malengo kadhaa yafuatayo:

  • Kudhibiti na Kuchunguza Mwenendo wa Imamu: Ma'mun, akitambua tishio la kisiasa lililotokana na shughuli za Imamu Ridha (a.s) mjini Madina, hivyo alilenga kumdhibiti kwa kumleta katika makao makuu ya utawala wake huko Merv na kumpa cheo cha urithi, na hivyo kumweka chini ya uangalizi wake. [12]
  • Kuzima Uasi wa Alawiyyuna: Uteuzi huo ulikuwa na lengo la kimkakati la kunyamazisha na kutuliza vuguvugu la uasi ulizokuwa ukiendeshwa na wafuasi wa  kizazi cha Imau Ali (a.s) (Alawiyyun). Bila shaka, baada ya uteuzi huo, hakukuwa na uasi mkubwa ulioibuka kutoka kwao, isipokuwa tukio dogo tu nchini Yemen. [13]
  • Kuchafua Taswira ya Imamu Mbele ya Mashia: Kulingana na ushahidi wa kihistoria kutoka kwa Abasalt, mfuasi wa karibu wa Imamu, ni kwamba; Ma'mun alidhamiria kumwonyesha Imamu (a.s), kama ni mtu mwenye tamaa ya mamlaka na anasa za kidunia, mkakati uliolenga kudhoofisha hadhi yake takatifu miongoni mwa wafuasi wake. [14]
  • Kujipatia Uhalali wa Kiutawala: Ma'mun alitambua wazi kuwa; Imamu Ridha (a.s) alikuwa na ushawishi mkubwa katika kuwaweka watu karibu naye, hivyo basi; kwa kumshirikisha katika utawala wake, alitaka kuhamisha uhalali wa ukhalifa wake, na hivyo kuufanya ukhalifa wake ukubalike mbele ya umma. [15]
  • Kutuliza Mkoa wa Khorasan: Mkoa wa Khorasan ulikuwa na idadi kubwa ya watu waliomuunga mkono Imamu Ridha baada ya kukatishwa tamaa na utawala dhalimu wa Bani Abbas.[16] Uteuzi huu ulikuwa ni hatua ya kisiasa ya kuwaridhisha na kuwatuliza. [17]
  • Kuwatambua Viongozi wa Kishia: Kwa kumweka Imamu (a.s) katika nafasi ya juu, Ma'mun alitarajia kuwa Mashia, ambao walikuwa  wakifanya shughuli zao kwa siri, wangelijitokeza hadharani. Hii ingeruhusu serikali ya Bani Abbas kuwatambua na kufuatilia mitandao yao. [18]

·        Kuongezeka kwa Nguvu za Ma'mun: Watu wa upande familia ya Abbas (Bani Abbas) walikuwa wakimdharau kiongozi wao Ma'mun. Sababu hasa ni kwamba; mama yake hakuwa malkia, bali alikuwa ni mtumwa (mjakazi) wa ikulu, na pia kwa uamuzi wake wa kuyakabidhi mamlaka yake  kwa Mwajemi (mtu kutoka Iran) aliyeitwa Fadhl bin Sahl. Kwa hiyo, Ma'mun alitaka kujiimarisha. Na akaamua kumchagua mtu maarufu na mwenye heshima kubwa, kama Ali bin Musa (a.s), ili awe mrithi wake. [19]

·        Wandishi wengine wanasema kwamba; Ma'mun alikuwa na sababu nyingine za kufanya hivyo. [20] Mtafiti wa historia anayeitwa Sayyid Ja'far Murtadha al-'Amili (ambaye ni Mshia) anaamini kwamba; Ma'mun alikuwa na matatizo mengi katika serikali yake. Kwa hiyo, kumchagua Imamu Ridha (a.s) kuwa mrithi wake, kunaonesha kwamba yeye alikuwa ni mjanja kisiasa, na anayajua matatizo yaliyokuwa yanaukabili uongozi wake. [21] Hata hivyo, inasemekana kwamba Imam Ridha (a.s.), kupitia maamuzi na misimamo yake, aliweza kupindua na kuharibu mipango iliyopangwa na Ma'mun, na kumfanya asiweze kufikia malengo yake aliyoyakusudia. [22]

Utendaji wa Imamu Ridha (as)

Maamuzi ya Imam Ridha Kuhusina na Urithi Mteule

Kwa mujibu wa maoni ya mwanazuoni aitwaye Sayyid Ja'far Murtadha al-'Amili, ni kwamba; riwaya zinazothibitisha kutokubali kwa Imamu Ridha (a.s) kushika wadhifa wa urithi wa ukhalifa (waliul 'ahd), ni Riwaya zinazokubalika na zenye daraja la mutawatir (zimepokewa kwa idadi kubwa ya watu, isivyowezekana watu hao wakubaliane katika urongo). [23] Kama ilivyonukuliwa katika kitabu kiitwacho Manaqib, Imam Ridha (a.s.), alikuwa ametoa ishara kuhusu ubatili na kutokuwa na tija juu ya urithi wake huo aliyopandikiziwa nao. [24] Kwa mujibu wa taarifa hii, baada ya kukubali rasmi wadhifa huo, Imamu (a.s) akiwa mbele ya Ma'mun na Fadhlu bin Sahl, aliandika waraka wa kisheria kuhusu urithi wake huo, ambapo alibainisha wazi kwamba; maarifa yaliyomo katika vitabu vya al-Jafr na al-Jami'ah (vitabu vya Hadithi kutoka kwa bwana Mtume), yanapingana na suala la yeye kuwa ni mrithi. [25]

Ma'mun, katika hatua ya awali kabla ya uteuzi wake wa kumteua Imamu (a.s) kama ni mrithi wa kiti cha ufalme, alimwasilishia Imamu Ridha (a.s) pendekezo la kumkabidhi madaraka ya ukhalifa. Hata hivyo, Imamu Ridha (a.s), alikana katakata pendekezo hilo kwa hoja ya kimantiki akisema: "Kama ukhalifa ni haki yako itokayo kwa Mungu, basi wewe huna mamlaka ya kumpa mtu mwingine. Na kama si haki yako, vipi basi utaweza kunatoa kitu usichokimiliki?" [26] Wanazuoni na watafiti mbali mbali wanaamini kwamba; jibu hili la Imamu (a.s.) lilidhoofisha na kuhoji (kuutikisa) msingi mzima wa uhalali wa utawala wa Ma'mun. [27] Sayyid Ja'far Murtadha anashikilia mtazamo usimao kuwa; Ma'mun hakuwa na dhamira ya kweli (hakuwa na nia safi) katika pendekezo lake la ukhalifa kwa Imamu Ridha (a.s.); bali ilikuwa ni mbinu ya kisiasa yenye lengo la kudhibiti na kuimarisha mamlaka yake. [28] Fadhlu bin Sahl naye alionyesha mshangao wake mkubwa kuhusiana na jinsi ya Ma'mun alivyokuwa tayari kuachia ukhalifa, na Imamu Ridha (a.s) akaukataa, jambo lililoashiria jinsi hadhi ya ukhalifa ilivyoporomoka (na kuchafuliwa na siasa). [29]

Pendekezo la wadhifa wa urithi wa ukhalifa (waliul 'ahd) lilipata upinzani mkali kutoka kwa Imam Ridha. [30] Pale Ma'mun alipokabiliwa na msimamo huo thabiti kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), aliamua kutumia mbinu ya vitisho, akirejelea tishio la kihistoria la Umar bin Khattab katika baraza la uteuzi wa watu sita, kwamba mpinzani yeyote yule atakayesimama dhidi ya maamuzi yake, angekabiliwa na adhabu ya kifo. Kitendo hichi kilimweka Imamu Ridha (a.s) katika hali isiyo ya hiari, na hivyo akashurutishwa kuukubali wadhifa huo. [31] Kwa mantiki hiyo, Imamu (a.s) alilazimika kukubali wadhifa huo, lakini aliweka sharti la msingi la kutojihusisha na nyanja zozote za utekelezaji wa mamlaka ya dola. [32] Ma'mun, kwa upande wake, alikubaliana na sharti hilo. [33] Kulingana na Riwaya iliyopokewa na Rayyan bin Salt kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), ni kwamba; kukataa kwake pendekezo hilo kungelisababisha kifo chake mikononi mwa Ma'mun. [34]

Ili kuhujumu mkakati wa Ma'mun kuhusiana na suala la urithi wa ukhalifa, Imam Ridha (a.s.) alitekeleza mikakati kadhaa ya kiupinzani katika nyakati tofauti. [35] Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na: agizo lake la kuiasharia familia yake, alilolitoa kwa kuonesha huzuni dhahiri wakati wa kuondoka kwake Madina, [36] kitendo cha kuaga kaburi tukufu la bwana Mtume (s.a.w.w), [37] kujiepusha kikamilifu na kutoshiriki katika masuala ya dola, na kuibadilisha nafasi yake ya utawala kuwa ni jukwaa la usambazaji wa fikra za Kishia na kuendesha midahalo ya kitaaluma na viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali. [38]

Safari ya Imamu kutoka Madina kwenda Merv

Kulingana na ripoti ya historia ya Ya'qubi, ni kwamba; kwa amri ya Ma'mun, Raja' bin Abi al-Dahhak (jamaa wa Fadhlu bin Sahl) ndiye aliyepewa jukumu la kumleta Imamu Ridha (a.s.) kutoka Madina hadi Khorasan. [39] Hata hivyo, kulingana na maelezo ya Sheikh Mufid, ni kwamba mjumbe wa Ma'mun aliyepewa jukumu hilo, alikuwa ni Isa Jaludi. [40] Ma'mun alichagua njia maalum kwa ajili ya safari ya Imamu Ridha (a.s.) kuelekea Merv, alifanya hivyo ili asipite katika miji yenye idadi kubwa ya Mashia, kwa sababu aliogopa kukusanyika kwao na kumzunguka Imamu (a.s.). [41] Alitoa agizo maalum ya kwamba Imamu (a.s.), asipitishwe kupitia njia ya Kufa, bali apelekwe Nishapur kupitia njia ya Basra, kisha Khuzestan hadi mji wa Fars, na hatimae aingizwe mji wa Nishapur. [42] Kulingana na kitabu cha Atlas ya Shia, njia ya safari hiyo ilikuwa kama ifuatavyo: Madina, Nuqrah, Hawsaja, Nabaj, Hafar Abu Musa, Basra, Ahwaz, Behbahan, Istakhr, Abarquh, Deh Shir (Farashah), Yazd, Kharanaq, Robat Posht Bam, Nishapur, Qadamgah, Deh Sorkh, Tus, Sarakhs, Merv. [43] Inasemekana kuwa; safari ya Imamu (a.s.), ilianza mwishoni mwa mwaka 200 Hijria. [44] Imeelezwa kuwa; tukio muhimu zaidi na lililothibitishwa zaidi katika safari nzima lilitokea Nishapur, ilikuwa ni kule Imam Ridha (a.s.) kutoa Hadithi maarufu inayojulikana kama Hadithi ya Silsilat al-Dhahab (Yenye Mnyororo wa Dhahabu), ambayo aliitoa kutika kuzungumzia mafunzo ya Tauhid (Upweke wa Mwenye Ezi Mungu). [45]

Hafla ya urithi wa kiti cha uongozi

Katika sherehe za kumsimika mrithi wa kiti cha ufalme, zilizofanyika Jumatatu, tarehe saba,[46] tano, [47] au mbili [48] ya mwezi wa Ramadhani mwaka 201 Hijria, Khalifa Ma'mun alipokea rasmi bay'a (kiapo cha utii) kutoka kwa umma kwa ajili ya kumtawadhisha Imamu Ridha (a.s.), kama ni mrithi wake. Tukio hili lilihusisha mabadiliko ya nembo ya utawala, ambapo mavazi meusi yaliyowakilisha nasaba ya Bani Abbas [49] yaliachwa na badala yake watu walitakiwa kuvaa mavazi ya kijani, yaliyokuwa ni nembo ya wafuasi wa Ali bin Abi Talib (a.s) (Alawiyyun). [50] Aidha, alitoa amri rasmi ya kiserikali ya kuutangaza uteuzi huo katika majimbo yote ya dola yake. [51]

Kufuatia uteuzi huo, mamlaka ya Imamu yalianza kutangazwa rasmi, ambapo hotuba za kidini (khutbah) zilitolewa kwenye mimbari kwa jina lake, na sarafu za dhahabu (dinari) na fedha (dirhamu) zilichapwa zikiwa na jina lake. [52] Ili kuimarisha uhusiano huo wa kisiasa, Ma'mun aliamua kumuoza binti yake, Umm Habib, kwa Imamu Ridha (a.s). [53] Vilevile, baadhi ya vyanzo vya kihistoria vinadokeza kuwa; Ma'mun ndiye aliyempa Imamu lakabu ya "Ridha" (Al-Ridha min Aali Muhammad, yaani, "Aliyeridhiwa kutoka katika Ukoo wa Muhammad") (s.a.w.w). [54] Hata hivyo, mtazamo huu unapingwa na mapokezi (Hadithi) mbali mbali za kidini kutoka kwa Imamu Jawad (a.s.), ambazo zinashikilia kuwa; lakabu hiyo ilikuwa ni tunuku ya Kiungu aliyotunukiwa baba yake na Mwenye Ezi Mungu. [55]

Ma'mun aliandaa sherehe maalumu kabisa, ambapo aliwakusanya maafisa wa serikali, makamanda wa jeshi, majaji na wananchi ili watoe kiapo cha utiifu kwa Imamu Ridha (a.s). [56] Imamu (a.s) aliweka mikono yake mbele ya uso wake, kwa mtindo wa Mtume wa kupokea kiapo cha utiifu; sehemu ya nyuma ya viganja vyake vikiwa vimeelekea usoni kwake, na viganja vyenyewe vikiwa vimekunjuliwa kuwaelekea watu. [57] Wahutubu na washairi walitoa hotuba na mashairi yao mbali mbali katika kuadhimisha sherehe hiyo. Mmoja wa washairi hao, alikuwa ni Di'bil al-Khuza'i, ambaye alipokea zawadi kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), baada ya kusoma shairi lake mbele yake (a.s). [58] Ma'mun alimwomba Imamu (a.s) atoe hotuba kwa ajili ya watu waliohudhuria hapo. Imam naye akatoa hotuba fupi sana kwa watu hao. [59]

Tangazo na agizo la kumfanya Imamu (a.s) kuwa ni mrithi liliandikwa kwenye hati husika kwa mwandiko wa Ma'mun mwenyewe. Imamu (a.s) naye aliandika mambo fulani nyuma ya hati hiyo. [60] Miaka mingi baadaye, mtu anayeitwa Ali bin Isa al-Irbili, aliyeandika kitabu cha Kashf al-Ghummah, alisema kuwa katika mwaka wa 670 (kwa kalenda ya Kiislamu), aliiona ile hati ya mkataba ikiwa na mwandiko wa Ma'mun na wa Imamu Ridha (a.s). Naye aliinakili hati hiyo na kuiweka kwenye kitabu chake hicho. [61]

Wapinzani wa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as)

Kulingana na mwanahistoria aitwaye al-Ya'qubi, ni kwamba; mtu mmoja aliyeitwa Ismail bin Ja'far bin Sulaiman, ambaye alikuwa mtawala wa mji wa Basra, alikataa kumuunga mkono Imamu Ridha (a.s). Hiyo Ma'mun akamtuma mtu aliyeitwa Isa bin Yazid al-Jaludi kumfuata, na Ismail akakimbia kutoka mji wa Basra. [62] Mwandishi huyo anasema kuwa; Isa al-Jaludi alikuwa amepewa kazi na Ma'mun ya kwenda Makka na kuwaambia watu wamuunge mkono Imamu Ridha (a.s). [63] Naye alienda Makka akiwa na vitambaa vya kijani na akawaamuru watu watoe kiapo cha kumkubali Imamu Ridha (a.s). [64] Lakini cha ajabu ni kwamba, mwandishi mwingine aitwaye Sheikh Saduq, anasema kwamba; baadaye, yuleyule Isa al-Jaludi alibadilika na kuwa mpinzani mkali wa Imamu Ridha (a.s). Hivyo Ma'mun akamweka jela kwa sababu hiyo ya kukataa kumuunga mkono Imamu (a.s). [65] Watu wengine waliopinga uteuzi huo wni pamoja na; Ali bin Abi Imran na Abu Yunus. [66]

Matukio

Baadhi ya matokeo ya uteuzi wa Imamu Ridha kuwa mrithi wa ukhalifa yameelezwa kama ifuatavyo:

  • Uasi wa watu wa Baghdad: Watu wa Baghdad, wakihofia kuwa ushawishi wao serikalini ungepungua kupitia uteuzi huo, waliamua kuukataa uteuzi wa kumteua Imamu Ridha (a.s) kama ni mrithi wa ukhalifa. Walimfukuza mwakilishi wa Ma'mun kutoka mji wa Baghdad na badala yake wakatoa kiapo cha utiifu wao kwa Ibrahim bin Mahdi. [67]
  • Kiapo cha utiifu cha baadhi ya wafuasi wa Imamu Ali (a.s): Ingawa uteuzi wa Imamu Ridha (a.s) haukuwafanya wafuasi wote wa Imamu Ali (a.s) kumuunga mkono Ma'mun, ila baadhi yao waliridhika naye na kuamua kumpa kiapo cha utii wao.[68]
  • Jinsi Imamu (a.s) alivyotumia fursa ya urithi: Licha ya kwamba Imamu Ridha (a.s) alikubali wadhifa huo bila kupenda, ila aliweza kutumia nafasi hiyo katika kuyafundisha mafunzo yake hadharani, ambayo hapo awali yalikuwa yakitolewa kwa wafuasi wake wa karibu na Mashia peke yao. Pia aliitumia fursa hiyo kwa ajili ya kufanya midahalo kadhaa na wanazuoni wa madhehebu mbalimbali. [69]
  • Kuandaa mazingira kueneza UShia nchini Iran: Kulingana maelezo ya Sayyid Ali Akbar Qurashi, mwandishi wa tafsiri ya Ahsan al-Hadith, ni kwamba; uteuzi wa Imamu Ridha uliandaa mazingira kwa Wairani katika kuuelewa na kuupokea Uislamu wa Kishia. Hii ni kwa sababu ya uwepo wa Imamu Ridha (a.s) nchini Iran, jambalo ambalo liliwafanya masharifu mbali mbali kuhamia huko na kueneza mafundisho ya Kishia nchini humo. [70]

Monografia

Kuhusu suala la urithi wa Imamu Ridha (a.s.), vitabu kadhaa maalum vimeandikwa, ambavyo baadhi yake ni hivi vifuatavyo:

  • Imam Ridha (a.s.), Ma'mun wa Maudhue Waliiahd (Imam Ridha (a.s.) Ma'mun na Suala la Urithi), kilichoandikwa na Sayyid Ghani Eftikhari: Katika kitabu hichi, mwandishi, pamoja na kuchunguza kipindi cha urithi wa Imamu Ridha (a.s), pia anachambua hali ya kisiasa na kijamii ya zama za ukhalifa wa Bani Abbas (za kabla ya Ma'mun). [71] Kitabu hichi kilichapishwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Behnashr Publications mwaka 2019 (1398 SHamsia) kikiwa na kurasa 152. [72]
  • Waliiahd Imam Ridha (a.s) (Urithi wa Imamu Ridha (a.s.)), kilichoandikwa na Muhammad Murtadhawi: Katika kazi hii kwa kurejelea vyanzo vya kihistoria, mwandishi anajaribu kuelezea malengo ya siri ya Ma'mun katika kumteua Imamu Ridha (a.s) kuwa mrithi wake, na jinsi Imamu alivyokabiliana na tukio hili. [73] Toleo la pili la kitabu hichi lilichapishwa mwaka 2007 (1386 SHamsia) na Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu kikiwa na kurasa 127 (Bunyade Pazuheshhaye Islami). [74]
  • Negahe Be Zindegi wa Waliiahdiy Imam Ridha (a.s) (Mtazamo wa Maisha na Urithi wa Imamu Ridha (a.s.)), kilichoandikwa na Mohammad-Ali Amini: Mada za kitabu hichi zimepangwa katika sura tatu, nacho ni kitabu chenye kurasa 130. [75] Kazi hii ilichapishwa na Behnashr Publications mwaka 2016 (1395 SHamsia). [76]

Rejea

Vyanzo